Jumanne 28 Aprili 2026 - 19:00
Mtazamo wa Imam wa Swala ya Ijumaa wa Baghdad kuhusu mabadiliko na vita vya kikanda

Hawza/ Ayatollah Sayyid Yasin Mousawi, akitoa tahadhari kuhusu “machafuko ya jumla” katika eneo yanayotokana na ushindani wa madola makubwa, alisisitiza kwamba; vita vijavyo vitabadilisha kwa msingi kabisa mizani ya nguvu.

Kwa mujibu wa ripoti ya Idara ya Kimataifa ya Shirika la Habari la Hawza, Ayatollah Sayyid Yasin Mousawi, Imam wa Swala ya Ijumaa wa Baghdad na mmoja wa walimu mashuhuri wa hawza ya kielimu ya Najaf Ashraf, katika khutba za Swala ya Ijumaa ya tarehe 24 April 2026, huku akiwasilisha uchambuzi wa mabadiliko ya Iraq, eneo na dunini kotea, alisisitiza kuwa: eneo lipo katika hali ya “machafuko ya jumla” yanayotokana na ushindani wa madola makubwa na athari zake kwa nchi za Mashariki ya Kati na Ulaya.

Mwanzoni mwa hotuba yake, alielezea hali ya kisiasa ya Iraq kuwa ni “tata na isiyotulia” na akasema: hali hii haiwezi kutenganishwa na vita kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Marekani na utawala wa Kizayuni. Mvutano huu umetanda juu ya eneo lote na umezikabili nchi za Ghuba ya Uajemi, Iraq, Syria, Misri, Yemen, Uturuki na hata Ulaya na aina fulani ya kukosekana kwa utulivu wa kisiasa na kiuchumi.

Imam wa Swala ya Ijumaa wa Baghdad pia, huku akirejelea hali ya uchumi wa dunia, aliongeza kuwa: kuyumba kwa bei za mafuta na athari zake kumesababisha shinikizo kwa mataifa, na jamii za Ulaya pia zinakabiliana na matatizo yanayoongezeka ya kisaikolojia na kijamii.

Ayatollah Mousawi katika sehemu nyingine ya hotuba yake kuhusu mabadiliko ya ndani ya Iraq, alisisitiza umuhimu wa kuepuka pupa katika maamuzi ya kisiasa na akaonya kuhusu shinikizo la Marekani. Alibainisha kuwa: uteuzi wa waziri mkuu unapaswa kuwa wa Kiiraq kikamilifu na mbali na aina yoyote ya kulazimishwa kutoka nje.

Mwalimu huyu wa hawza ya Najaf pia huku akirejelea suala la kuzuia uhamishaji wa baadhi ya rasilimali za kifedha za Iraq, aliitaja hatua hii kuwa ni “chombo cha shinikizo la kisiasa” kwa ajili ya kudhoofisha uhuru wa maamuzi katika nchi hii, na alidai kuwa: Marekani haina nia ya kuona kiongozi mwenye ufanisi na uadilifu akichukua uongozi wa serikali ya Iraq.

Imam wa Swala ya Ijumaa wa Baghdad aliendelea kukosoa mpango wa “huduma ya kijeshi ya lazima” uliowasilishwa katika Bunge la Iraq, na akasema; kwa kuzingatia hali ya sasa ya kiuchumi na kiusalama, kuwa ni “usiotekelezeka”.

Akirejelea uwepo wa vikosi vikubwa vya kijeshi na usalama nchini Iraq, vyenye idadi inayokadiriwa kufikia watu milioni moja na laki mbili, aliongeza: kuongeza vikosi bila mipango ya kimkakati hakuhalalishiki.

Ayatollah Mousawi alisisitiza: watu wa Iraq katika nyakati nyeti wamekuwa wakilinda nchi yao bila ya kuhitaji sheria za kulazimishwa, na uzoefu wa kupambana na kundi la kigaidi la Daesh ni ushahidi wa jambo hili.

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, alirejelea taarifa ya mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa nchi za Kiarabu kuhusu Iran, na akazitaja baadhi ya tuhuma zilizotolewa kuwa ni “zisizo na ushahidi wa kweli”, na akazitathmini katika muktadha wa upangaji wa misimamo ya kisiasa.

Imam wa Swala ya Ijumaa wa Baghdad pia alidai: baadhi ya nchi za eneo kwa kutoa vituo vyao vya kijeshi, zimejihusisha katika migogoro, na majibu ya Iran pia yamelenga vituo hivyo.

Akiikosoa nafasi ya Saudi Arabia katika mabadiliko ya eneo, alizungumzia kile alichokiita “mpango wa kihistoria wa kutawala kisiasa”, na akarejelea baadhi ya matukio ya kihistoria yanayohusiana na kuundwa kwa tawala za eneo pamoja na mabadiliko ya Iraq, Lebanon na Syria.

Ayatollah Mousawi aliendelea kwa kutoa wito kwa nchi za eneo kufanya mapitio ya mahusiano yao na Marekani, na akapendekeza mfumo unaotegemea ushirikiano wa kikanda kati ya Iran, Uturuki na Pakistan uwe mbadala wa utegemezi kwa madola ya nje.

Alionya kuwa: kuendelea kwa utegemezi wa kisiasa kunaweza, endapo vita vipya vitatokea, kusababisha “mgogoro mpana” katika eneo, na akaongeza kuwa: maendeleo ya kijeshi na kiteknolojia, hasa nchini Iran, yanaendelea kubadilisha mizani ya nguvu.

Mwisho, Imam wa Swala ya Ijumaa wa Baghdad alisisitiza kwa kusema: utulivu wa eneo unaweza kupatikana tu chini ya kivuli cha uhuru na maamuzi yanayotokana na mamlaka ya kitaifa, na nchi za eneo zinapaswa, kwa kuelewa unyeti wa hali, kuepuka kuingia katika migogoro ambayo si kwa manufaa ya mataifa yao.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha